CHAMA cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), leo kitafanya mkutano mkubwa wa hadhara
katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam ambapo Mwenyekiti wake,
Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Wilbord Slaa watahutubia.
Aidha,
viongozi wengine wakiwemo wabunge wake 15 ni miongoni mwa watakaoshiriki
mkutano huo, akiwemo Mbunge wa Ubungo John Mnyika ambaye juzi, alitangazwa na
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa mbunge halali baada ya kushinda kesi
ya kupinga ushindi wake, iliyokuwa ikimkabili.
Joto la
mkutano huo limepanda kiasi kwamba, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, limetangaza kuweka ulinzi mkali.
Taarifa ya
CHADEMA jana imesema kuwa, ingawa Mahakama Kuu imewapatia ushindi wabunge wake,
Tundu Lissu, John Mnyika, Gervas Mbasa na wengine waliopingwa, leo katika
mkutano huo itaeleza umuhimu wa mabadiliko ya kimfumo katika mhimili huo, na
katika utendaji kazi wa Tume ya Uchaguzi (NEC), ambayo chama hicho kinataka iwe
chombo huru katika kutekeleza majukumu yake nyeti mbalimbali, ikiwemo kusimamia
uchaguzi.
Akizungumza
na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika,
alidai kunahitajika mabadiliko ya kimfumo kwa sababu kumekuwa na athari kubwa
katika maendeleo ya wananchi, na pia kikwazo cha kuweka madaraka ya uendeshaji
wa nchi mikononi mwa umma kama inavyotamkwa katika ibara ya 8 ya katiba ya
sasa.
“Tunataka
wananchi wajitokeze kwa wingi kusikiliza masuala mbalimbali, zikiwemo hoja juu
ya umuhimu wa kufanya mabadiliko ya kimfumo kupitia uandikwaji wa katiba mpya,
waje wajue namna ambavyo ubovu wa katiba ya sasa umechangia kwa kiasi kikubwa
matatizo makubwa yanayotukabili kama taifa,
ikiwemo umaskini, ujinga, maradhi, ufisadi na CCM yenyewe,” alisema Mnyika.
Alidai kuwa
katika mkutano huo, watazindua kampeni ya ‘kuiamsha Dar es Salaam’, ikiwemo kaulimbiu ya ‘Vua
Gamba, Vaa Gwanda’ inayotarajiwa kuwapokea viongozi na wanachama wengi kutoka
CCM.
Aliongeza
kuwa, tofauti na CCM ambayo imeanza mchakato wa katiba kwa kujifungia na kutoa
misimamo ya mamlaka za chama bila hata maoni ya wanachama wake nchi nzima,
CHADEMA itatumia fursa hiyo kutoa elimu ya uraia kwa umma juu ya sheria ya
mabadiliko ya katiba, ili kuwezesha umma kumiliki mchakato na hivyo taifa
lipate katiba bora.
Mbali na
Mnyika, wabunge wengine watakaoonekana leo ni pamoja na Peter Msigwa, Ezekiah
Wenje, Tundu Lissu, Grace Kiwelu, Halima Mdee, Rose Kamili, Mhonga Said, Suzan
Kiwanga, Joyce Mkya, Godbless Lema na Meya wa Manispaa ya Musoma, Alex Malima
Kasurula.
MVUTANO
POLISI, CHADEMA
Hata hivyo,
pamoja na Jeshi la Polisi kuruhusu kufanyika kwa mkutano huo, kumezuka mvutano
kati ya pande hizo mbili kuhusu suala la wanachama kufanya matembezi ya hiyari
kutoka kila kona ya Jiji la Dar es Salaam kuelekea Jangwani.
Wakati
CHADEMA wakitangaza ramani yatakapopita matembezi hayo, polisi imeyapiga
marufuku kwa madai kwamba hakuna sheria yoyote inayoruhusu chama cha siasa
kufanya matembezi au maandamano.
Awali,
CHADEMA ilituma maombi ya maandishi kwa Jeshi la Polisi kuruhusu matembezi hayo
ya amani, kutoka sehemu mbalimbali za jiji hadi viwanja vya Jangwani
panapofanyika mkutano wa hadhara leo.
Lakini jana
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema,
wanaruhusu kufanyika kwa mkutano huo, na wamejiandaa kikamilifu katika ulinzi,
lakini si kwa matembezi.
Kwa mujibu
wa Kamanda Kova, CHADEMA iliwasilisha barua ya kuomba kibali cha kufanya
mkutano, lakini kabla ya kujibiwa, kilipeleka barua nyingine yenye lengo la
kupewa kibali cha matembezi ya amani.
Kova alidai
kuwa, mwanachama yeyote atakayekaidi amri hiyo, atachukuliwa hatua za kisheria,
na kuonya kuwa watu wasidanganyike kufanya matembezi hayo, ila kila mtu anayo
haki ya kwenda katika mkutano kwa namna ya kawaida.
Hata hivyo,
CHADEMA imepinga na kudai kuwa hayo si maandamano, bali matembezi maalum kutoka
kwenye maeneo ya jiji kwenda viwanja vya Jangwani, ikizingatiwa kuwa hali ni
ngumu na si kila mtu mwenye uwezo wa kumudu gharama za usafiri.
Chama hicho
kimedai kuwa, Watanzania wanayo haki kikatiba kufanya maandamano na mikusanyiko
ili mradi hawavunji sheria, na kimetangaza barabara zitakazotumiwa na watu wa
majimbo ya Ilala, Ukonga na Segerea, kuwa ni Buguruni, Uhuru, Msimbazi,
Morogoro hadi Jangwani.
Watakaotoka
majimbo ya Kinondoni, Kawe na Ubungo, watakutanika katika bustani ya Magomeni,
kupitia barabara ya Morogoro hadi Jangwani, wakati wale wa Kigamboni, wataanzia
Kivukoni, kupitia Posta ya zamani, Makao Makuu ya Jiji, barabara ya Morogoro
hadi Jangwani.
Wale wa
Temeke, wataanzia Mwembeyanga, kupitia barabara ya Mandela, Buguruni na
kukutana na wale wa majimbo ya Ilala na kuelekea Jangwani.
PEOPLEEEEE!
ReplyDeleteZZZ POWERRRRRR
ReplyDelete