Thursday, May 31, 2012

JAMII

Jamii Yetu Itambue, Ithamini Umuhimu Wa utamaduni Wa Lugha



LUGHA ya Kiswahili ni sehemu ya utamaduni wa Mtanzania, ambao unaweza kumtambulisha  popote ulimwenguni. Hii ni kutokana na ukweli kwamba hivi sasa  lugha hii imekuwa na mashiko katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, hata hivyo watu wa mataifa ya  nje ya Afrika, wanatambua ni lugha hii kutoka Tanzania.

Kwani utamkaji tofauti tofauti wa vitamkwa vya Kiswahili kwa wazungumzaji wa lugha licha ya kuwa na lahaja moja iliyosanifishwa katika eneo la ukanda huu, lakini Watanzania kwa asilimia kubwa ndio wanaomudu kuzungumza Kiswahili fasaha.

Wapo watu mbalimbali wanaopenda kujifunza lugha ya Kiswahili, ili waweze kuimudu vyema kama ilivyo kwa lugha  mama zao, ambazo hizo wanazungumza kwa ufasaha. Kwa jumla, kufahamu lugha mbalimbali ulimwenguni ni jambo la msingi hasa kwa wanadiplomasia, ina tija katika hilo ili kujenga uhusiano mwema kwa mataifa husika wanayoshirikiana nayo.

Hii ni sawa unapokwenda katika eneo la mbali na ukaweza kuwasiliana na jamii utakazozikuta huko kwa lugha zao za asili. Hiyo inaweza kusaidia kufahamu kwa urahisi mambo mbalimbali katika jamii hiyo.

Ndiyo maana wakoloni na hata wamisionari  walipofika Bara la Afrika, waliweka msukumo katika kujifunza lugha za wenyeji na kufanikisha azma yao kwa urahisi.

Itakumbukwa wiki iliyopita, taifa letu lilikuwa linasherehekea jubilei ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara), ambapo kabla ya kufikia kilele pale  Desemba 9, taifa lilipokea salamu za pongezi  kwa sherehe hizo, ambazo zilitumwa na viongozi mbalimbali akiwamo Rais Barack Obama wa Marekani, ambapo salamu zake hizo alizotuma kwa Rais, alidiriki kutumia lugha ya Kiswahili, akinukuu maneno kama Mungu awabariki. Ni jambo jema kwa viongozi  maarufu duniani kuendelea  kutambua nafasi ya Kiswahili.

Siyo hayo tu hivi karibuni katika uga huo wa Kiswahili tumeshuhudia waimbaji wa Ambassador of Christ kutoka Rwanda, walikuja nchini kwa ajili ya uzinduzi wa albamu yao pia  wakikimudu vyema Kiswahili katika utunzi wa nyimbo katika albamu hiyo na kuweza kuteka soko la muziki wa injili kwa na kuwavutia wapenzi wa muziki aina hiyo.

Kwa maana nyingine hayo ni matunda ya Jumuia ya Afrika Mashariki, ambapo nao wameamua kuchangamkia fursa ya kuuza kazi zao za Kiswahili nchini.

Mathalani, katika kuangalia soko la ushindani katika Kiswahili, pia  hivi sasa  wapo wageni kutoka China ambao wameanza kutafiti Watanzania wanapenda nini na kuweza kutengeneza baadhi ya bidhaa, hata kwa kujaribu kuweka majina ya Kiswahili kama vile simu, vyombo vya ndani na nguo ili kuweza kuwavutia wanunuaji wa bidhaa hizo.

Vilevile, katika televisheni ya TBC1 tumeshuhudia Kiswahili kimeendelea kuchangamkiwa, kwa namna ambavyo Wachina  wametumia tamthilia yao ambayo imetafsiriwa kwa Kiswahili, ili kuwaburudisha watazamaji.

Hayo yote ni namna wenzetu wanavyobuni ili kujinasibu na jamii ya Waswahili, waweze kuuza bidhaa mbalimbali zao kazi zao za sanaa ili  waweze kunufaika kiuchumi.

Hayo yote yakiwa yanaendelea pia hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete, aliwakumbusha viongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) katika kuangalia fursa za kutangaza fursa mbalimbali za utalii nje ya Tanzania na kuwaasa viongozi hao, kuangalia vyanzo mbalimbali ambavyo wanaweza kuvitangaza nje ya nchi, ili kuongeza idadi ya watii wa ndani.

Kauli hiyo inapaswa kuungwa mkono kwani kwa namna moja au nyingine zipo fursa mbalimbali za kukuza Kiswahili kwa njia ya utalii; kupitia matangazo mbalimbali na wageni wanaweza kuja kujifunza lugha hiyo.

Pia,  katika kutangaza vivutio vya ndani njia hiyo inaweza kusaidia kutangaza utamaduni wetu wa lugha, kuliingizia taifa fedha za kigeni.

Kwa nafasi ya wanasiasa pia  wanayo nguvu ya kuendelea kuwahimiza  jamii kuthamini utamaduni wetu, tunapoanza kujiandaa kuadhimisha jubilei nyingine miaka ijayo, ama baada ya miaka ishirini na tano, hamsini, sabini na tano au mia moja, ili taifa letu liweze kusimama kama taifa lenye utamaduni imara  wa lugha.

Hata hivyo, wasomi waliopo wa ngazi ya shahada na uzamili wanayo nafasi ya kuendelea kuchangia makala na kuweka midahalo, ambayo itawaelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuuthamini utamaduni wa  lugha pamoja na kuandika vitabu vinavyo husiana na  utamaduni wa lugha.

Hii inatokana na ukweli kwamba kasi ya uandishi wa vitabu kwa jumla hasa katika maudhui ya ujenzi wa  jamii, imepungua kutokana na jamii kutokuwa na mwamko wa kusoma vitabu vya watu wengine na watu wengi kujikita katika harakati za kujitafutia mlo wa siku.

Ni vyema taasisi za lugha ya Kiswahili kwa Tanzania Bara na Zanzibar zikaweka mikakati yake katika  kupeleka mbele gurudumu la maendeleo katika  Kiswahili na jamii kutambua umuhimu wa utamaduni wa lugha ya Kiswahili.

Pia, kuwasaidia wenye taaluma za Kiswahili, wakaona matunda ya kuchagua fani hiyo kwa kunufaika kwa kupata fursa za ajira pamoja na kutoa udhamini wa kuchapa vitabu vya kitaaluma.

Katika kufanikisha hayo, dhamira ya dhati iwekwe katika kuendeleza kizazi cha sasa, ili nao waweze kuwa walimu wazuri kwa wenzao kwa kizazi kijacho.

Hivyo katika kuhakikisha Kiswahili kinaendelea kupata heshima katika uga mbalimbali ipo haja ya kuwa na kozi fupi, ambazo zitawasaidia watu wa rika mbalimbali kuwa na mbinu za uwasilishaji wa mada katika hadhara ya watu.

Kwa mfano, wazungumzaji wa Kiswahili kufahamu mbinu za uwasilishaji wawapo katika midahalo, darasani na sehemu nyingine za kitaaluma.

Kwa kufanya hivyo itasaidia wageni kuendelea kushawishika kujifunza Kiswahili kwa kuwa hilo ni eneo ambalo linaonyesha taswira ya Kiswahili kwa mtu yeyote anayependa kujifunza lugha hiyo, kufahamu uzuri wa utamkaji wa vitamkwa kwa ufasaha na ufundi wenye mvuto.

JAMANI!:..hivi katika jamii yetu kuna kazi za kike na za kiume?

 

Shukrani za dhati zikufikie kwa kuamua kuwa mmoja wa wasomaji wa makala hii ya Darasa huru ambayo kila Jumamosi huwa inakujia, ikiwa na lengo moja kubwa zuri la kukuelimisha na kukufanya uwe mzoefu na mwenye hekima katika maisha yako ya kila siku.

haitoki nje ya humu, ..kiukweli, kinachojadiliwa humu ni kitu ambacho kila siku unakutana nacho na leo nimeamua kujadili mambo ambayo katika jamii zetu tumeanza kuyachukulia kana kwamba ni mambo ya aibu!

Kuna kazi jamani watu wanaziita kwamba ni kazi za kike au kuna kazi watu wanadai kabisa kwamba mtoto wa kiume ukionekana unafanya kabisa kabisa unaweza kudharaulika na jamii. Usiniambie hujawahi kukutana na haya mambo na kama ushawahi kukutana nayo, ilikuwaje?

Busara ulikuwa nayo ama na wewe ulikubaliana na hili?

Si unajua kuna haya mambo ya kuosha vyombo, kubeba mtoto, kufagia uwanja, kuteka maji na kadhalika, nasikia kwamba mtoto wa kiume akionekana anafanya hizi kazi anaweza kabisa kuchekwa na vijana wenzake, kwa sababu moja tu inayoaminika kuwa kubwa na ya msingi, ya kwamba hizi ni kazi kwa ajili ya wanawake tu.

sasa katika kichwa changu, chenye uwezo mdogo wa kufikiri npengine kuna mambo nimeyafikiria na nimeyaweka katika mafungu kama kawaida, tufuatane na tujue mwisho utakuwaje?

1. Nani kasema?

nataka kujua hii dhana imetoka wapi? Hii ya kwamba kuchota maji sijui, kuosha vyombo, kubeba mtoto mgongoni na hata kupika wakati mwingine, nani alisema kwamba hii ni kazi kwa ajili ya wanawake tu na akikutwa mwanaume anafanya hizi kazi ni kosa. Ni nani alianzisha hili au lilionekana wapi? Au watu tu wamejiamulia na wakakubaliana kwamba hii ni hivi.

Ujue bwana sisi huku mtaani kwetu tuna dhana moja, tukiona watoto wanachezea matairi, basi tunaanza kuamini kwamba kuchezea matairi ni mchezo wa kitoto lakini kumbe hata mtu mzima unaweza kulitumia tairi katika kufanya mazoezi ya kukimbia.

Mnanielewa wenzangu na mie?

kwa hiyo hata hizi kazi zinazoitwa za kike huenda watu kwa sababu wameona wanawake wanazifanya sana basi wameamua kuamini kwamba hizi ni kazi za kike na mwanaume akifanya hizi basi anadharaulika kumbe inawezekana kuna siku moja huyu mwanamke ambaye tunamtegemea akaja akapata matatizo ya kibinadamu na akasaidiwa hizi kazi na mwanaume bila huyu mwanaume kuwa na wasiwasi nwowote.

Au sio jamani?

Maana mwanaume sasa hivi amekuwa muoga hata kumsaidia mwanamke mtoto, kumbeba ile mgongoni wakati mwingine anakuwa anahisi kwamba akifanya ile kazi, wanaume wenzake wakimuona wanaweza kumshushia heshima yake kwa hiyo mwisho wa siku kuna mambo yanashindikana kwenda vizuri pale mwanamke anapokuwa na udhuru.

2. Akili ya kupewa, changanya na yako...

Kuna mambo mengi, tumezaliwa , tumeyakuta na tunaishi nayo lakini mengi kila tukiyaangalia tunakuja kugundua kwamba kwa wakatio huu tulionao, hatuna budi kuachana nayo maana dunia imekwenda hatua nyingine moja na tukiamua tubaki hapa tulipo tutakuja kujikuta tuna hasara kubwa sana kimaendeleo.

...niamini mimi!

Ningekuwa na uwezo wa kukushauri jambo kaka ama dada yangu, ningekwambia hivi, katika hii dunia ya sasa, akili yako ndio inategemewa sana katika kuleta maendeleo yako wewe mwenyewe, usitegemee akili za watu kukuongezea maisha yako.

Sawa ndg yangu?

Sio kila utakalolikuta duniani, basi na wewe ulifuate ndg yangu, kuna mambo mengine si sawa kwako. sasa usije hata siku moja ukafanya jambo eti kwa sababu fulani kafanya, au umekuta watu wanafanya kwa hiyo na mimi nafuata mtiririko huo.

..hapo unakuwa unakosea.

Nakuomba sana zingatia hili, akili za kupewa, changanya na zako.

No comments:

Post a Comment