TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mei 25, 2012
TAIFA STARS, MALAWI UWANJANI
DAR
Timu za Taifa za Tanzania (Taifa Stars) na Malawi (The Flames) zinapambana kesho (Mei 26
mwaka huu) katika mechi ya kirafiki itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa
10 kamili jioni.
Makocha wa timu zote mbili, Kim
Poulsen wa Taifa Stars na Kinnah Phiri wa The Flames wamezungumzia umuhimu wa
mechi hiyo katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika leo (Mei 25 mwaka
huu) ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kim ambaye hiyo itakuwa mechi yake
ya kwanza tangu asaini mkataba wa kuinoa Stars, amesema baada ya mazoezi ya
siku kumi hicho ndicho kipimo chake cha kwanza na cha mwisho kabla ya kucheza
na Ivory Coast kwenye mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia itakayofanyika ugenini
Juni 2 mwaka huu.
“Wachezaji wangu wamekuwa wakipokea
mafunzo vizuri ingawa Nurdin Bakari na Thomas Ulimwengu hatakuwepo kwa vile ni
majeruhi. Bila shaka baada ya mazoezi ni lazima ujipime, hivyo mechi hii ni
muhimu kwangu ukizingatia kuwa kwenye ubora wa viwango vya FIFA, Malawi wako juu
yetu,” amesema Kim.
Naye Phiri ambaye ni mchezaji wa
zamani wa kimataifa wa Malawi
amesema awali aliombwa mechi na Misri, lakini akaamua kucheza na Taifa Stars
kwa vile anaamini kitakuwa kipimo kizuri kwake kabla ya kucheza mechi ya mchujo
ya Kombe la Dunia dhidi ya Kenya
itakayofanyika Juni 2 mwaka huu jijini Nairobi.
“Nimekuja na wachezaji 20 ambapo
nusu yao wanacheza mpira wa kulipwa nje ya Malawi, wengi wakiwa Afrika Kusini lakini wapo
pia kutoka Msumbiji na mmoja anacheza Hispania katika timu ya vijana ya
Atletico Madrid.
Tumejianda si kwa mechi hii tu, bali pia dhidi ya Kenya
na baadaye Nigeria
ambao tutacheza nao numbani Juni 9 mwaka huu,” amesema Phiri ambaye kwenye
benchi lake la ufundi anasaidiwa na Young Chimodzi.
Viingilio katika mechi hiyo ni sh.
3,000 kwa viti vya kijani, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000
kwa VIP C na B wakati VIP A inayochukua watazamaji 748 tu itakuwa sh. 20,000.
ASHANTI, POLISI KUFUNGUA LIGI YA TAIFA
Michuano ya Ligi ya Taifa
inayoshirikisha mabingwa wa mikoa inaanza Mei 27 mwaka huu katika vituo vitatu
tofauti huku Ashanti United ya Ilala na Polisi ya Mara zikifungua dimba katika
Kituo cha Musoma.
Ligi hiyo ambayo inatarajia
kumalizika Juni 12 na 13 mwaka huu itashuhudia mechi mbili kwa siku katika kila
kituo, huku ya kwanza ikichezwa saa 8 mchana na kufuatiwa nay a pili 10 jioni.
Mechi za ufunguzi Kituo cha Musoma
ambapo mechi zake zitachezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma ni
Flamingo ya Arusha dhidi ya Forest ya Kilimanjaro (saa 8 mchana) wakati saa 10
jioni ni Ashanti
United na Polisi.
Kituo cha Kigoma siku ya ufunguzi
kutakuwa na mechi moja tu itakayoanza saa 10 kamili jioni kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika kati ya Mwadui ya Shinyanga na JKT
Kanembwa ya Kigoma. Siku inayofuata ni CDA (Dodoma) vs Majimaji ya Tabora (saa 8 mchana)
na Bandari ya Kagera vs Pamba ya Mwanza (saa 10 kamili jioni).
Tenende ya Mbeya na Kurugenzi ya
Iringa ndizo zitakazoanza saa 8 mchana kwenye Kituo cha Mtwara na kufuatia na
mechi kati ya Mpanda Stars ya Rukwa na Ndani ya Mtwara kuanzia saa 10 kamili
jioni. Mechi hizo zitachezwa katika Uwanja wa Umoja.
HALI YA MAMBO NDANI YA YANGA
Kwa vile wajumbe kadhaa wa Kamati ya
Utendaji ya Yanga akiwemo Mwenyekiti wa kamati hiyo Lloyd Nchunga wamejiuzulu,
Kamati ya Uchaguzi ya Yanga imeliandikia barua Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) ikitaka mwongozo juu ya hilo.
Kwa kuzingatia hilo,
TFF imepeleka suala hilo kwa kamati yake ya
Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ili itoe maoni yake kisheria ya nini
kinafanyike kuhakikisha Yanga inaendelea na shughuli zake kama
kawaida.
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi
za Wachezaji chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa inatarajia kukutana leo
jioni kushughulikia suala hilo
na baadaye Kamati ya Uchaguzi ya Yanga pamoja na Kamati ya Uchaguzi ya TFF
zitapewa maelekezo ya kufanya kwa kuzingatia taratibu zilizopo.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment