Ujio wa
Nape: Kagera Tumedharauliwa na Uzalendo Umedhihakiwa
Tumejaribu
kutafakari kwa kina juu ya nini hasa kilimsukuma Nape kufika Kagera na
kushiriki mazishi ya muasisi wa TAA, mzalendo na mpigania uhuru aliyetelekezwa
na Taifa lake, Dr. Vedasto Kyaruzi na bado ki-ukweli hatujapata majibu.
Tunapata
shida kujua dhima ya safari ya Nape kwa kuwa shughuli mahsusi alizozifanya
akiwa Kagera zina kinzana kimaadili na kitamaduni na maombolezo ya misiba ya
Kiafrika na hasa misiba ya Kihaya. Mjumbe aliyetumwa mahsusi toka mbali
kupeleka pole kwenye msiba hategemewi atumie muda wake mwingi majukwaani
kufanya siasa, tena katika mazingira ya ugenini lakini kwenye maeneo yale yale
msiba unapoendelea. Kwa mpita njia ambaye amefahamishwa tukio na akahiari
kufika msibani, akiendelea na shughuli zake haitakuwa ajabu na hakuna mtu
mwenye akili timamu atamshangaa hata kidogo.
Nape
aliingia Bukoba tarehe 25/05/2012. Na ni uungwana kukiri kuwa alifika
Kashai-Matopeni msibani kutoa salamu za pole. Lakini baada ya hapo alielekea
Missenyi ambako tunaarifiwa alikuwa na mikutano ya hadhara. Watanzania
mtakumbuka vema kuwa katika mikutano hiyo ndiko Nape alitoa kauli ya kutokuwa
tayari kukabidhi nchi kwa wahuni! Labda ili Watanzania muweze kupima vema
uelewa na akili za Nape, tuwafahamishe kuwa Missenyi ndiko iliko Kyaka na
ambako maziko ya Dr. Kyaruzi yamefanyika. Tunashindwa kuelewa, hiyo mikutano
ilikuwa safisha njia ya mazishi au inahusiana vipi na mtu aliyepeleka ujumbe wa
maombolezo?
Linalochanganya
zaidi ni hili la Jumamosi tarehe 26/05/2012. Hii ndiyo siku ambayo Dr. Kyaruzi
alipumzishwa rasmi kaburini alale kwa amani. Lakini kwa Nape akiwa Kyaka hii
ilikuwa siku maalumu ya kufungua matawi na kutangaza operation yake mpya ya
kisiasa iitwayo “Vua Gamba, vua Gwanda, Vaa Uzalendo”. Katika hili, ukiachilia
ukinzani wa matukio kimaadili na kitamaduni, tunapata mishangao mingine; hivi
Nape alikwenda Kyaka kuzika au kuzindua operation ya kisiasa? Na Je, huyu
kijana anahubiri uzalendo upi? Uzalendo usiokuwa na utamaduni, Uzalendo wa
kuwatelekeza na kushindwa kuwaenzi watu waliopigania uhuru wa nchi hii? Kama huo ndiyo uzalendo anaohubiri Nape, basi hauhitaji
operation wala kampeni maana tayari tunao magwiji. Na hapo kwa tafsiri hii,
ujio na matukio ya Nape kwenye maeneo ya msiba huu vinanapata maana halisi.
Katika
Taarifa ya Uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, Chama Tawala kimearifiwa kuwa
moja ya kosa lililofanyika ni kumteua mgombea ambaye mila hazikuwa zinampa
fursa na tafsiri njema kufanya shughuli kama
ya siasa katika muda mfupi baada ya msiba wa Baba yake. Ikiwa kosa hili la
Kitamaduni limechangia Chama kupoteza Jimbo, basi pia chama kiwe tayari kwa
makosa ya Nape kupoteza zaidi ya Kijiji cha Burifani na Kata nzima ya Kyaka. Na
hatutoshangaa iwapo Nape au Taasisi iliyomtuma ikishindwa kuomba radhi!
Mbali na
vioja vya Nape hapo juu, kwa wasifu wa marehemu Dr. Kyaruzi, kila mmoja
atakubaliana nasi kuwa Taasisi yoyote (iwe dola au chama) kuwakilishwa na mtu
wa ngazi ya Nape ni dharau ya hali ya juu na ichukuliwe ni dhihaka si kwa jamii
iliyostaharabika tu, bali hata kwa watu walipendao Taifa lao na kuuenzi
Uzalendo. Inakuwa vigumu kuamini kuwa pamoja na ugumu wa ratiba, Rais alikosa
muwakilishi makini wa hadhi inayobeba uzito sawia na mchango wa Dr. Kyaruzi katika Taifa hili. Tukio
hili linaleta hisia za ubaguzi wa Taasisi za dola na chama katika kutoa uzito
kwenye majanga, matatizo na misiba ya watu wa Taifa hili. Ni majuzi tu Taifa
lilipotelewa na Mcheza Sinema nguli ambaye hapo awali hakuwahi kupata heshima
yoyote ya Kitaifa. Lakini tuliona jinsi viongozi wa Serikali na Chama
walivyohamia msibani na Serikali kujipa jukumu la kuubeba msiba na shughuli za
mazishi. Haikupita muda, Rais akiwa ziarani Marekani, Rais wa Malawi alifariki duniani. Pamoja na
uchovu wa safari tulimwona Rais akiingia nchini na kutoka kuwahi mazishi ya
Rais wa nchi jirani. Kulingana uzito na umuhimu uliowekwa na Rais katika msiba
huu, hakusubiri hata atatue matatizo makubwa yaliyokuwa yanaikabili serikali
yake kiasi cha kutishiwa kuanguka. Lakini pia ni kawaida kusoma taarifa za Rais
anazoandika katika mitandao ya kijamii (MyKj) kila anapoelekea kwenye misiba ya
watu wa kawaida walioko katika maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam. Hili
linatuongezea huzuni na kutuongoza kuamini kuwa misiba ya watu wa maeneo nje na
Dar es Salaam haigusi hisia za Rais hata kama ni ya Watu waliotoa mchango mkubwa kwa Taifa hili.
Haya yaliyotokea kwa Dr. Kyaruzi alimanusura yatokee pia kwenye msiba wa MKUU
wa Majeshi Mstaafu Jenerali Ernest Mwita Kyaro. Marehemu Mwita alifariki siku
chache baada ya mazishi ya Kanumba na msiba wake ulikosa sura ya Kitaifa.
Isingekuwa kelele za wana-Mitandao ya Kijamii (MyKj) na wahandishi wa habari,
hata Bunge lisingesimama kwa dakika moja kutoa salamu. Tabia hii ya kutelekeza
wazalendo wa Taifa hili inaonekana kumea kwa kasi. Na uthaminisho wa serikali
kwa watu wa Dar es Salaam
unaonekana kuwa juu kuliko wa wale walioko nje ya Dar es Salaam.
Kwa Tamko
hili tunamtaka Nape Nnauye, Katibu Mwenezi wa CCM kama
kweli alikuja kuwakilisha Taasisi yoyote katika msiba wa Dr. Kyaruzi, basi aiombe radhi jamii
yetu kwa dharau kubwa aliyoonyesha katika msiba huu. Na kama alikuwa mpita njia
tu, basi atujuze ili Jamii na historia ya Taifa imwandike rasmi Dr. Kyaruzi
kama muasisi wa TAA na mzalendo aliyepigania uhuru wa Taifa lake ambaye
hakuenziwa wakati wa uhai wake na hata mazishi yake hayakuhudhuriwa na mwakilishi
wa Kitaifa.
Na mwisho
tunamtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania,
yeye kama Taasisi awe Rais wa Watanzania wote; wa Dar es Salaam na Mikoani.
Asiye na
Utamaduni ni Mtumwa. Tanzania
ni Moja
Imetolewa
na:
Erick
Mwemezi Kimasha
Mhamasishaji
Jamii Mkuu
Vijana wa
Bukoba Mjini Waishio Dar es Salaam
Barua Pepe:
ekimasha@ksgroup.co.tz
Simu:
0713-177-372
Tarehe:
27/05/2012
No comments:
Post a Comment