Saturday, May 26, 2012

WAANDISHI wa habari Zanzibar

WAANDISHI wa habari Zanzibar wametakiwa kubadilika katika uandishi wao
kwa kuandika habari zinazogusa zaidi maslahi ya jamii badala ya kuandika
habari za kupamba viongozi na watu maarufu nchini.

Imefahamika kuwa kuna habari nyingi za kuziandikia zenye maslahi na jamii ya
Zanzibar ambazo zitakapojulikana kunaweza kupelekea mabadiliko makubwa
katika jamii jambo ambalo litachochea maendeleo na kasi ya uwajibikaji.

Wito huo umetolewa na Mshauri wa Wanahabari Zanzibar Salim Said Salim
wakati wa mafunzo ya siku nne iliyofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari
Maelezo Zanzibar, juu ya uandishi bora na namna ya kuzingatia maadili.

Salim amesema miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakigusa hisia za
wazanzibar ni pamoja na uingizwaji wa bidhaa mbovu ambazo zinapelekea
wananchi kuwa na shaka katika matumizi na hata kupata maradhi mbalimbali.

Amesema kama waandishi watakuwa wakitekeleza kazi zao vizuri na kuweza
kufichua masuala kama hayo Zanzibar haitaweza kuingizwa bidhaa hizo mbovu
na wale ambao watafanya hivyo wataweza kufichuliwa na kuchukuliwa hatua
kwa mujibu wa sheria za Nchi.

Hivyo waandishi wa habari ni watu muhimu katika jamii kwani kalamu yao
wakiitumia vizuri kwa maslahi ya nchi basin nchi inaweza kupiga hatua za haraka
sana na mambo maovu kama hayo na mengineyo hayataweza kutendeka.

Amewasisitiza waandishi kujiamini katika kazi zao kwa kuzingatia maadili ya
taaluma yao ambayo ndio muongozo katika kutekeleza kazi zao vizuri bila ya
kujali habari hizo imemgusa nani.

Akifunga mafunzo hayo Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar
Yussuf Omar Chunda amewataka waandishi hao kutekeleza yale yote
waliyoyapata katika mafunzo hayo ili kutoa habari zenye kuvutia.

Amesema kuwa anaamini kuwa Taaluma waliyoipata itasaidia Taifa na
kuwajengea hadhi waandishi na taasisi zao ili ziwe zinakubalika na jamii.

Chunda amesema kuwa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar itaendelea kutoa
mafunzo kwa waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini viwe vya
Serikali au binafsi kwani vyombo hivyo vyote ni vya Zanzibar na vinahudumia
Wazanzibari hivyo niwajibu wote kupata elimu ya habari ya kisasa

Mafunzo hayo ni ya pili kutayarishwa na Idara ya habari Maelezo Zanzíbar na
yakwanza yalifanyika Jijini Dar es Salaam mwezi wa Machi mwaka huu ambayo
yalikuwa yamejikita katika uandishi wa habari za kibiashara na uchumi

No comments:

Post a Comment